Vikosi vya jeshi la Syria vimewatimua waasi waliokuwa wakiizingira jela
kuu ya Aleppo tangu mwaka mmoja uliopita.Ushindi huu umejiri wiki mbili
tu kabla ya uchaguzi utakaomthibitisha rais Bashar al Assad madarakani.
Ushindi huo wa vikosi vya jeshi la serikali umejiri pia masaa machache
kabla ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuupigia kura mswaada wa
azimio lililowasilishwa na Ufaransa kutaka korti ya kimataifa ichunguze
madai ya uhalifu wa vita nchini Syria.Jeshi la Syria likisaidiwa na vkosi vya ulinzi wa taifa-FDN,wanamgambo wa Hisbollah wa kutoka Libnan na wapiganaji wengineo wa kiarabu limefanikiwa kuivunja ngome ya waasi waliokuwa wakiizingira kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa jela kuu ya mjini Aleppo-kaskazini ya Syria.
Mkurugenzi wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam nchini Syria,lenye makao yake makuu nchini Uingereza Rami Abdel Rahmane amethibitisha ripoti hizo.Akizungumza na waandishi habari bwana Rami Abdel Rahman amesema vifaru viliingia katika uwanja wa jela hiyo na risasi kufyetliwa mtindo mmoja kabla ya vikosi vya kawaida vya jeshi kuwasili katika eneo hilo.Watu 50 wanasemekana wameuwawa miongoni mwa waasi.Hasara upande wa vikosi vya serikali bado haijulikani.Waasi waliokuwa wakiizingira jela hiyo walikuwa wamepania kuwafungua wafungwa elfu nne wengi wao wa makosa ya jinai.
Ukurasa mpya katika medani ya mapigano
Ushindi wa jeshi la Syria katika eneo hilo la kaskazini unapelekea kufungwa njia muhimu ya kupatiwa misaada waasi kutoka maeneo wanayoyadhibiti na lile linalopakana na Uturuki.
Kwa mujibu wa gazeti linaloelemea upande wa serikali,Al Watan, ushindi wa vikosi vya jeshi la serikali "utafungua ukurasa mpya katika medani ya mapigano".Ushindi huo utasaidia kuimarisha udhibiti wa mji huo na hasa katika mitaa inayokaliwa na makundi ya watu wenye silaha na kulazimisha kufikiwa makubaliano sawa na yale yaliyofikiwa Homs".
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius akizungumza na maripota wa magazeti ya Wall Street Journal la Marekani na Le Monde la Ufaransa amelisihi baraza la usalama la umoja wa mataifa liunge mkono mswaada wa azimio ili korti ya kimataifa ikabidhiwe jukumu la kuchunguza uhalifu wa vita nchini Syria.Urusi imeshasema itatumia kura yake ya turufu kuupinga mswaada huo ambao balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vitali Tchourkine ameulinganisha na "Mbio za sakafuni."
No comments:
Post a Comment