Dk Shein akataa kuongeza posho BLW
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari
imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote
kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.
Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohamed Shein amekataa maombi ya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000.
Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.
Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha
jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho
ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini
kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu
imeshindikana kufanya hivyo.
Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na
subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo
linaweza kufikiriwa.
Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na
Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi
kuhusu suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao
vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa
mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo
itakapotengamaa,” alisema Hamad.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari
imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote
kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh 150,000
kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000
kwa mwezi.
Akizungumzia kikao cha bajeti kinachoanza leo
mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika kupunguzwa kwa
siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na linatarajiwa
kukutana Agosti 5.
Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti
kinatarajia kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na
muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda na kuwahi
Bunge la Katiba.
Aidha, katibu huyo wa BLW alisema kikao hicho
kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya
Fedha na ule wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka
2014/2015.
Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema
SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati
ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi
kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment