Wednesday, May 14, 2014

ATAKAYEKACHA MAFUNZO JKT KUSHTAKIWA

Atakayekacha mafunzo JKT kushtakiwa


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange (kulia), Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Samuel Ndomba (katikati) na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Raphael Muhuga wakisoma kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 


Dodoma. Vijana wasiopungua 45,000 watakaomaliza kidato cha sita watajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na watakaokwepa mafunzo hayo ya miezi mitatu, watashtakiwa.
Mpango huo wa kupitisha JKT wahitimu wa kidato cha sita na vyuo, ambao ulifutwa mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na matatizo ya kifedha na kurejeshwa bila mafanikio ya miaka ya hivi karibuni, ulilenga kujenga uzalendo kwa vijana na kuongeza ukakamavu.
Jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk Hussein Mwinyi alisema utaratibu huo ni wa kisheria na si hiari, hivyo wahitimu wa kidato cha sita watambue kuwa ni kosa kukaidi wito wa kujiunga na JKT.
Dk Mwinyi, aliyekuwa anawasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, vijana watakaojiunga na jeshi watafanya hivyo kwa awamu tatu.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha vijana 20,000 ambao wataingia katika mafunzo hayo Juni hadi Septemba 2014 na kufuatiwa na wa awamu ya pili itakayochukua vijana 14,450 kuanzia Oktoba hadi Januari 2015 wakati awamu ya tatu ya vijana 10,550 itaanza Januari hadi Aprili 2015.
Hata hivyo, kumekuwepo na mwingiliano wa muda wa kujiunga na jeshi hilo na wa kujiunga na masomo ya juu. Kati ya vijana 15,000 waliotakiwa kujiunga na jeshi hilo kati ya Oktoba 2013 na Januari 2014, waliojiunga walikuwa 1,002 tu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano huo, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alisema atatoa ufafanuzi huo leo.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alitaka mafunzo ya JKT kwa wabunge yafanyike kwa miezi miwili hadi mitatu badala ya wiki mbili.
Bulaya, ambaye alipitia mafunzo hayo pamoja na wabunge wenzake wakati mpango huo uliporejeshwa mapema mwaka jana, alisema kuwa hali hiyo itawafanya wabunge hao kujifunza mambo mengi zaidi.
Bulaya aliwataja baadhi ya wabunge vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa ni John Mnyika (Chadema-Ubungo) na Catherine Magige (viti maalumu-CCM).
“Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu wabunge kwenda kwenye mafunzo kwa miezi miwili hadi mitatu,” alisema na Bulaya na kuongeza:
“Katika kambi za JKT kuna tatizo la vifaa vya afya, hivyo wizara iliangalie hilo ili wanaokwenda katika mafunzo hayo wapate tiba sahihi na kwa wakati.”

No comments:

Post a Comment