- Mshtakiwa huyo kabla ya kumbaka, alimwekea Kitabu kitukufu cha Quran kichwani na kumwambia kuwa kwa aya anayomsomea, akimweleza mtu kitu atakachomfanyia atageuka kipofu.
Liwale. Mahakama ya Wilaya ya
Liwale, Lindi imemhukumu Mussa Chande kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa
la kumbaka mtoto wa miaka 11 anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi
Kawawa.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama
ya Wilaya Liwale, Eric Ruhumbiza alimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo
chini ya Kifungu namba 130 na 131 vya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana
(Sospa) ya mwaka 1998.
Ruhimbiza alisema Mahakama imeridhishwa na
ushahidi uliowasilishwa na upande wa mlalamikaji mahakamani hapo na
kumtia hatiani pasi na shaka yoyote mshtakiwa kwani ushahidi uliotolewa
na shahidi namba tano ambaye ni binti aliyebakwa ambaye alitoa maelezo
ya maumbile na viungo vya siri vya mtuhumiwa ulitosheleza.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, PC Josephat
alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 8, mwaka huu saa nne asubuhi
ndani ya Msikiti wa Kawawa, Liwale jirani kabisa na shule anayosomea
mwanafunzi huyo.
Alisema mshtakiwa alimchukua mtoto huyo na
kumwingiza msikitini, sehemu wanayosalia wanawake na kumlaza chini na
kumvua nguo huku akimfunika kwa kanga usoni.
Aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo kabla ya
kumbaka, alimwekea Kitabu kitukufu cha Quran kichwani na kumwambia kuwa
kwa aya anayomsomea, akimweleza mtu kitu atakachomfanyia atageuka
kipofu.
Alisema jambo hilo lilifahamika baada ya
mfanyabiashara katika na eneo la shule hiyo kutilia shaka nyendo za
mwalimu huyo wa dini kuingia kwenye msikiti upande wa wanawake na kutoka
kila mara kuchungulia nje.
Alisema mfanyabiashara huyo alipofuatilia, alikuta
mwanafunzi huyo akitoka msikitini huku akilia na alipomhoji alimweleza
kilichojiri ndipo alipoomba msaada kwa wanawake waliokuwa jirani.
Alisema wanawake hao walimchukua na kumwogesha
kisha wakampeleka hospitalini. Alisema uchunguzi ulipofanyika katika
eneo la tukio, mbegu za kiume zilionekana pamoja na kanga.
Mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama impe adhabu
kali mshtakiwa kwani licha ya tendo ovu la kumbaka na kumdhalilisha
mtoto huyo, aliudhalilisha Uislamu na kitabu kitakatifu cha Quran
kufanikisha uhalifu wake.
No comments:
Post a Comment