Boko Haram ni magaidi wa kimataifa - UN
Baraza la usalama la umoja wa
mataifa hatimaye limeidhinisha kuwekewa vikwazo kundi la Boko Haram
baada ya utekaji nyara wa takriban wasichana 300 wa shule katika eneo la
Chibok Nigeria.
Kundi hilo limeshutumiwa kuwaua maelfu ya watu nchini Nigeria katika miaka michache iliyopita.Nigeria ni mwanachama wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa kipindi cha miaka miwili. Kwa nafasi hii imeweza kushinikiza baraza hilo kuimulikia tochi.
Vikwazo na adhabu
Hatua ya baraza hilo kuiorodhesha Boko Haram miongoni mwa magaidi wa kimataifa, wakipishana au hata kuhusishwa moja kwa moja na AL Qaeda, huenda isionekane kama hatua kubwa. Lakini hii ina maana kuwa sasa jamii ya kimataifa italichukulia kwa uzito mkubwa zaidi kundi hilo.Baraza hilo limeidhinisha pia vikwazo kuwekewa kundi hilo, viongozi wake na yeyote anayehusishwa nalo. Hii ina maana kuwa hata mali zao zitazuiliwa na akaunti zao zote zinazojulikana kufungwa.
Jamii ya kimataifa
Mjumbe wa Marekani katika Umoja wa mataifa Samantha Power amepongeza hatua hiyo akisema kuwa itaimarisha vita vya serikali ya Nigeria dhidi ya Kundi hilo, ambalo limetikisa jamii ya kimataifa mwezi uliopita kwa kuwateka zaidi ya wasichana mia mbili wa shule.Kwa upande wake mjumbe wa Australia katika baraza hilo balozi Gary Quinlan amesema kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa Boko Haram wamepewa mafunzo na kundi la Al Qaeda hasa namna ya kujitengenezea mabomu, mtindo ambao umekuwa mbinu mpya zaidi ya ugaidi
No comments:
Post a Comment